Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018, na kutaja shule 10 zilizofanya vizuri katika mtihani huo kwa shule zenye watahiniwa zaidi ya 40.
Katika matokeo hayo mwanafunzi aliyefanya vizuri zaidi ni kutoka shule ya sekondari Ilboru ya Arusha, anaitwa Hope Mwaibanje.
Isikupite hii: Matokeo ya kidato cha nne 2018/2019. Tazama hapa
Akitangaza matokeo hayo leo Alhamisi Januari 24, 2019 mkoani Dodoma, Katibu Mkuu wa Baraza, Dk. Charles Msonde amezitaja shule hizo kuwa ni St Francis Girls (Mbeya), Kemebos (Kagera), Marian Boys, Ahmes, Marian Girls (zote Pwani), Canossa, Bright Future Girls (zote Dar es Salaam), Maua Seminari (Kilimanjaro), Precious Blood (Arusha) na Bethel Sabs Girls (Iringa).
Amesema watahiniwa tisa wasichana kati ya 10 bora kitaifa, katika matokeo haya ni kutoka Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Francis ya Mbeya, huku msichana wa 10 bora kitaifa, anatoka shule ya Wasichana ya Anwarite ya Kilimanjaro.
Katika matokeo hayo, watahiniwa 252 wamefutiwa matokeo kutokana na udanganyifu na kati yao, 71 ni wa kujitegemea huku wawili kati yao wakiandika matusi.